Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland amekwepa adhabu kutoka Chama cha Soka cha England (FA) kwa kosa la kumzonga mwamuzi Simon Hooper baada ya kusimamisha mchezo kwenye mechi dhidi ya Tottenham iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 Jumapili (Desemba 03).
Mshambuliaji huyo alionesha kukasirika kwa kutuma video na uamuzi wa Hooper kushindwa kumruhusu Jack Gealish kuwahi pasi dakika za nyongeza za mchezo huo.
Chanzo kutoka FA kiliambia ESPN kuwa video hiyo ya Haaland haikuvunja sheria yoyote inayohusiana na matamshi ya kwenye vyombo vya habari.
Haaland, ambaye pia anaongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu ya England pia alikwepa rungu la kumzonga Hooper kufuatia maamuzi yake yaliyomzuia Grealish kuwahi mpira kwenye mechi hiyo.
Tukio hilo lililowahusisha Haaland na Hooper ndilo lililosababisha Manchester City ipigwe faini na FA kwa kuvunja kanuni ya E20.1 inayohusu vitendo vya wachezaji wao.
Haaland aliongoza kundi la wachezaji wenzake wakiwemo Ruben Dias na Mateo Kovacic, kumzongoa Hooper wakipinga maamuzi yake.
Taarifa ya FA ilisema: “Manchester City imehukumiwa kwa uvunjifu wa kanuni ya FA E20.1 baada ya wachezaji wake kumzonga mwamuzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Tottenham Jumapili iliyopita.
“Inadhaniwa kuwa kwenye dakika ya 94, klabu ilishindwa kuwazuia wachezaji wake kumzonga mwamuzi.
“Manchester City imepewa mpaka Desemba 7 kujibu kuhusiana na hukumu hiyo.”