Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa inatarajia kuanzisha huduma ya sheli zinazotembea ‘Mobile Pump Station’ kwa kutumia magari maalumu yaliyotengenezwa kwa kazi hiyo zikiwemo pikipiki za miguu mitatu zinazoendelea kuundwa kupitia chuo kikuu cha Dar Es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano wa mamlaka hiyo, Taitas Kaguo wakati wa semina elekezi juu ya ufanyaji kazi wa mamlaka hiyo iliofanyika mkoani Njombe huku akitambulisha ofisi mpya ya kanda iliyopo mkoani Mbeya.
Amesema kuwa nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika, hivyo kujenga visima vikubwa ni gharama ndio maana wamekuja na njia hiyo mpya ambayo itarahisisha usambazaji wa nishati hiyo kwa wananchi.
Aidha, amesema katika maeneo mengi hapa nchini wafanyabiashara wadogo wadogo wamekuwa wakisafirisha na kuuza mafuta kwa njia ambazo sio sahihi na zinazohatarisha usalama wa vyombo vya watumiaji pamoja na maisha yao wenyewe lakini hasa maeneo ya vijijini ambako hakuna vituo vya mafuta.
‘’Ewura tumejitahidi kukomesha tatizo la uchakachuaji wa mafuta ambalo lilikuwa limekithiri siku chache zilizopita lakini sasa limekwisha baada ya kutumia njia ya vinasaba vya rangi pamoja na kupitia uagizaji wa mafuta kwa pamoja katika meli moja,’’amesema Kaguo
Pia ameshauri watumiaji vya vyombo vya moto kuacha kujaza mafuta katika vyombo vyao majira ya mchana kwa kuwa kuna kiasi cha mafuta hupotea kwa njia ya mvuke na kupelekea malalamiko ya kuwa wananyonywa na wahudumu au wamiliki wa vituo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kusafirisha au kuuza mafuta kwa njia zisizo rasimi kwa kutumia madumu ni kosa kisheria na pia hatari kubwa inayoweza kusababisha majanga kama milipuko ya moto.
-
Mpina apiga marufuku makongamano ya kumpongeza JPM
-
Majaliwa azitaka benki kupunguza riba za mikopo
-
EWURA kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Chiristopher Ole Sendeka amewapongeza Ewura kwa kuanzisha ofisi za kanda ambazo zitahudumu mikoa ya Njombe ,Ruvuma, Mbeya, na Katavi.