Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ameiagiza TUGHE- Taifa kueleza juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu masuala ya Wafanyakazi akitolea mfano upandishwaji madaraja wa mseleleko kwa watumishi ambao hawajapanda madaraja kwa muda mrefu.

Amewataka pia kuwashirikisha wanachama wao ili kuisaidia Serikali katika kupeleka maendeleo kwa wananchi na pia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake kwa Wafanyakazi, huku pia akiipongeza EWURA kwa kupitia upya gharama za uagizaji wa mafuta ambazo amesema kuwa, awali zilikuwa kubwa na zilikuwa zikipelekea athari mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa gharama katika Sekta ya Usafirishaji na Uzalishaji.

Dkt. Biteko alitoa agizo na pongezi hizo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika hii leo Novemba 8, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.

Amesema, “gharama hizi za uagizaji mafuta zilikuwa kubwa mno huku kukiwa hakuna sababu ya kuwa kubwa kwa kiasi hicho, niliwapa maelekezo mkazitazame upya, nashukuru mmeziangalia na ninafurahi kwamba zimeshuka na hivyo kupunguza makali kwa watumiaji.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa, Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi lengo likiwa ni kuhakikisha Huduma za Nishati na Maji zinapatikana kwa uhakika, kwa kutosha, kwa uendelevu na kwa gharama ambazo wananchi wanazidumu.

Alimshukuru, Dkt. Biteko kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi hiyo na miongozo anayotoa ambayo inafanya EWURA iendelee kuboresha utendaji wake katika kuhudumia Watanzania.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA kinachoendelea jijini Dodoma kimelenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Bajeti ya EWURA kwa mwaka 2022/2023 na Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za EWURA za mwaka 2022/23.

Mkude: Ubingwa bado sana Young Africans
Dkt. Biteko aitaka EWURA kudhibiti urasimu, rushwa