Masoud Kipanya, mbunifu aliyetengeneza gari linalotumia nishati ya umeme ameweka wazi gharama alizotumia kulikamilisha gari hilo pamoja na ukubwa wa timu yake.
Kipanya ameanika kiasi cha fedha alichotumia kukamilisha mradi huo, alipofanya mahojiano maalum na Dar24 Media kwenye studio za chombo hicho cha habari.
Mzamiru: Hatma ya Simba ni Jumapili
Awali mbunifu huyo ambaye pia ni mchoraji wa vibonzo na mtangazaji wa redio, alielezea ukubwa wa timu ya wataalam waliohusika katika kulisuka gari hilo kwa kipindi cha miezi 21 baada ya kuwakabidhi mchoro wenye vipimo na mahitaji.
“Nina welder (mchomelea vyuma) ana wasaidizi wawili, nina wapaka rangi wawili, nina msimamizi mmoja, kuna mpiga picha ambaye anarekodi kila kitu. Unajua sisi Lambat (mtangazaji) kila siku tunarekodi kila tunachofanya,” Kipanya aliiambia Dar24 Media.
Aliendelea kueleza kuhusu ujira aliokuwa akiwalipa wafanyakazi wake saba kwa siku.
“Kwahiyo nina jumla ya watu saba. Sitakuficha, hawa watu sita nawalipa Sh.10,000 kila mmoja kwa kila siku. Na mtu mmoja namlipa Sh. 20,000. Kwahiyo, kwanza kuna Sh. 80,000 ya kila siku ya kazi,” alisema.
Muwekezaji huyo alifafanua kuwa mbali na gharama hizo, kuna gharama za chakula, gharama za kodi ya eneo la kazi ambayo ni Sh. 460,000 kwa mwezi, bado hajaweka gharama za umeme, vifaa, ukarabati wa eneo la kazi na mengineyo. Lakini kwa gharama hizo tu kwa miezi 21 ya kazi iliyofanyika alitumia Sh. 75 Milioni.
“Hii Sh. 75 Milioni kwa miezi 21 hapa sijaweka ‘material’ ambayo nilikuwa narudia mara kwa mara pamoja na gharama nyingine nyingi. Maana yake ni kwamba niliwekeza muda na fedha lakini kitu kilichotoka pale hata nikiondoka leo mimi najua mtasema Masoud alituanzisha safari,” Mbunifu na mtangazaji huyo wa Clouds Radio alifunguka kwenye ‘Exclusive ya Dar24’.
Angalia mahojiano kamili hapa: