Kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mzamiru Yassin amesema mchezo Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barabni Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, utaamua hatma ya klabu yao kutinga Nusu Fainali ama la.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo utakaounguruma Jumapili (April 17) Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wakiwa na matarajio makubwa ya ushindi kwa timu yao.

Mzamiru amesema matokeo ya mchezo huo yakiwa mazuri yatakua njia salama kwa Simba SC kupambana ugenini katika mchezo wa Mkondo wa Pili, utakaorindima Afrika Kusini Jumapili (April 24).

Amesema malengo makubwa ya Simba SC msimu huu, ni kucheza Nusu Fainali ya Michuano ya Kimataifa yanayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, baada ya kuishia Robo Fainali katika Ligi ya Mabingwa mara mbili (Msimu wa 2018/19 na 2020/21).

“Mchezo wetu wa kesho kutwa (Jumapili-April 17) ndio utakuwa wa hatma kwa maana tunahitajika kushinda magoli mengi zaidi, Malengo yetu msimu huu ni kufika hatua ya nusu Fainali ya kombe la shirikisho.” Amesema Mzamiru Yassin.

Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kishindo, baada ya kuibanjua USGN mabao 4-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (April 03), matokeo yaliyoifanya klabu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, ikitanguliwa na RS Berkane ya Morocco.

Simba SC ilifikisha alama 10 sawa na RS Berkane, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikipata alama 09 na USGN ya Niger ikikusanya alama 05 zilizoiweka mkiani mwa kundi hilo.

Rais Samia afanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani
Moses Phiri: Naweza kubaki Zambia msimu ujao