Kocha wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi ameanza kufungua faili lake la mbinu kali kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Gamondi ameendelea kuwaongezea dozi ya mazoezi wachezaji wake ambapo kwa sasa wanafanya mara mbili kwa siku.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Young Africans, zinaeleza benchi la ufundi chini ya kocha huyo limefanya tathmini kubwa kuelekea katika mchezo huo baada ya kuwasoma wapinzani wao kupitia mikanda ya video na kuamua kubadilisha programu zake kwa lengo la kuwaongezea utimamu wa kutosha wachezaji wake kabla ya mchezo huo.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo katika benchi la ufundi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema Kocha baada ya kuangalia mikanda ya wapinzani wake kuna kitu alikibaini na kuamua kuongeza dozi hiyo ya mazoezi.
Unajua Kocha alitoa mapumziko mwishoni mwa juma na ndiyo maana Jumatatu tulianzia ufukweni kwa ajili ya wachezaji kurudisha utimamu wao kabla ya kurejea uwanjani kuendelea na ratiba zengine za kiufundi, amebaini wapinzani wetu wana nguvu hivyo ameamua pia kuwaongezea stamina wachezaji wetu” amesema kiongozi huyo.
Amesema Gamondi na benchi lake la ufundi wanajua wanachokitaka baada ya kuwangalia wapinzani, hali iliyomlazimu kubadilisha programu kwa kuongeza muda zaidi wa kufanya mazoezi kulingana na ukubwa wa mchezo uliopo mbele yao kwa sasa.
Amesema Young Africans imepania kutinga hatua ya makundi na ndio sababU wanapanga mikakati yao vizuri na kuwasoma wapinzani wao kabla ya kukutana katika mechi mbili zitakazoamua timu yao kusonga mbele.
Wakati Young Africans watasafiri kwenda Rwanda kuifuata Al Merrikh ambao wamechagua kuchezā mchezo wao wa nyumbani nchini humo Septemba 17, Simba SC itasafiri mpaka Zambia kuumana na Power Dynamos ya nchini humo Septemba 16 kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Michezo ya marudiano ambayo itafanyika jijini Dar es salaam inatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 29 na 30 mwaka huu.