Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kesho Jumapili watakua na kazi ya kutimiza ndoto zao za kutwaa mataji matatu kwa msimu mmoja, pale watakapopapatuana dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) mjini SUmbawanga, Rukwa.
Mpambano huo utakaounguruma kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga, utashuhudia Simba SC wakiwa na kumbukumbu ya kushinda Ngao ya Jamii na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema wanahitaji kumaliza fainali hiyo ‘mapema’ ili kukamilisha malengo yao ya kutwaa kikombe cha tatu msimu huu na cha pili chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.
Matola amesema wachezaji na benchi la ufundi wako tayari na mchezo huo ambao hautakuwa na presha kubwa kwa sababu tayari timu zote mbili (Simba na Namungo), zimeshakata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.
“Tulifika Sumbawanga tangu juzi jioni, na leo jioni tutafanya mazoezi mepesi ya mwisho, kila mchezaji anajua tunahitaji kurudi na ushindi, ingawa tumewaambia Namungo ni timu nzuri na yenye wachezaji wenye kasi, tunahitaji kuthibitisha ubora wetu wa msimu mzima,” alisema Matola.
Ameongeza hakuna mchezaji majeruhi na alimtaja nyota Tairone Santos ndiye aliachwa Dar es Salaam kwa sababu bado hajawa fiti tangu alipoumia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC mjini Ruangwa, Lindi uliochezwa mapema mwezi uliopita.
Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Thierry Hitimana, amesema kikosi chake kimejiandaa kukutana na ushindani kwa sababu watacheza dhidi ya timu bora na yenye wachezaji wenye uzoefu wa michezo ya michuano mbalimbali.
“Ni mchezo mkubwa, lakini fainali huwa haina mwenyewe, ukitumia vema nafasi na kujaribu kupunguza makosa, una nafasi nzuri ya kupata ushindi, tunamuomba pia Mungu awe upande wetu, tunahitaji kushinda na kupata kikombe hiki cha kwanza msimu huu,” amesema Hitimana.
Amewataja wachezaji wake waliokuwa majeruhi akiwamo Blaise Bigirimana na Reliant Lusajo wameimarika na atawatumia katika fainali hiyo ambayo kwa timu yake ni mafanikio makubwa.
Simba SC walitinga fainali ya michuano ya ASFC baada ya kuwafunga Azam FC katika mchezo wa hatua ya robo fainali na baadaye kuwaondoa Young Africans kwenye hatua iliyofuata kwa kuwapa kichapo cha mabao manne kwa moja.