Rais wa Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Amani Karume amezungumzia fursa na haki ya Kikatiba ya kugombea urais wa Zanzibar na kama ana mpango wa kuitumia hivi karibuni.
Akizungumza wiki hii kwenye Mahojiano na Times Fm, Mwanasheria huyo alijibu swali la mtangazaji aliyetaka kufahamu kuhusu tetesi alizodai ziko mtaani kuwa ana mpango wa kugombea Urais wa Zanzibar.
Akijibu swali hilo, Fatuma ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Mjukuu wa Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, Sheikh Abeid Amani Karume, alisema kuwa hana mpango wa kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, Bi. Fatma alifafanua kuwa endapo akiamua kugombea nafasi hiyo, hakuna mtu atakayemzuia.
“Hapana! Sina ndoto hiyo, lakini nikitaka nitafanya. You can’t stop me my friend, none of you can stop me (huwezi kunizuia rafiki yangu, hakuna kati yenu anayeweza kunizuia).
“Na hao waliokwambia kwamba nina hiyo ndoto, waambie hivi it is my constitutional right (ni haki yangu ya kikatiba). Mimi ni Mzanzibar, nimezaliwa Zanzibar, nina haki nikitaka kugombea Urais wa Zanzibar… ni haki yangu,” aliongeza.
Bi. Fatma ambaye hueleza kuwa sio mwanachama wa chama chochote cha siasa, alichaguliwa Aprili 14 mwaka huu kuwa Rais wa TLS kwa kipindi cha mwaka mmoja.