Aliyekua kiungo wa kutumainiwa wa FC Barcelona Xavi Harnandez amempigia chepuo mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC Paulo Dybala, ili asajiliwa Camp Nou mwishoni mwa msimu huu.
Xavi, ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Qatar, amesema Dybala ana vigezo vyote vya kuwa mchezaji wa FC Barcelona na amemfuatilia kwa muda mrefu, na kubaini ana uwezo mkubwa ambao utaweza kuisaidia klabu hiyo ya Cataluña.
“Ni mchezaji mahiri na mkakamavu, anafaa kuwa miongoni mwa watakaoitetea Barcelona msimu ujao, ningependa kuona anasajiliwa Camp Nou ili aongeze nguvu katika safu ya ushambuliaji. Ana kila sababu ya kupewa sifa ya kupambana, kwa sababu ameonyesha uwezo mkubwa akiwa na Juventus. Amesema Xavi.
Wakati Dybala akipigiwa chepuo la kuelekea FC Barcelona, Real Madrid nao wanatajwa kuwa katika mpango wa kumfuatilia mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina na huenda mwishoni mwa msimu huu wakatuma ofa Juventus Stadium.
Mpaka sasa Dybala ameshaifungia Juventus mabao 27 katika michezo 56 aliyocheza, tangu aliposajili mwaka 2015 akitokea Palermo.