Mabingwa wa La Liga FC Barcelona wametozwa faini ya EURO 300 sawa na dola za kimarekani 328, baada ya kubainia walikwenda kinyume na taratibu za usajili wa Antoine Griezmann.
Kamati ya mashindano ya shirikisho la soka nchini Hispania RFEF, limeendesha kesi iliyomuhusu mshambuliaji huyo kwa muda wa wa miezi miwili, baada ya uongozi wa Atletico Madrid kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya FC Barcelona.
Atletico Madrid waliilalamikia FC Barcelona kuvunja taratibu za usajili, kwa kufanya mazungumzo na Griezmann akiwa bado na mkataba na klabu hiyo ya mjini Madrid, jambo ambalo ni kinyume kanuni.
Kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na kamati ya mashindano ya RFEF, imebainika ni kweli FC Barcelona walitenda kosa hilo, hivyo wameadhibiwa kwa kutozwa faini ya EURO 300, na kutakiwa kutorudia tena kosa kama hilo.
FC Barcelona walimsajili Griezmann kwa ada ya EURO milioni 120 mwezi Julai mwaka huu.