Shirikisho la kabumbu Tanzania TFF, limethibitisha litaanza kutoa mgawo wa fedha zilizotolewa na Shirikisho la Kandanda duniani FIFA, kwa wanachama wake mbalimbali ikiwamo klabu za Ligi Kuu Bara ili kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyia jana mjini Sumbawanga mkoani rukwa, Rais wa TFF Wallace Karia, alisema mgawo huo utakwenda pia mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mitano iliyoko Zanzibar.
Karia alisema pia fedha hizo za Fifa zitagawiwa kwa klabu za Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, Ligi Kuu ya Wanawake na vyama shiriki vyote vinavyotambuliwa na TFF.
Kiongozi huyo alisema kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kimeridhia kuanza kwa ujenzi wa vituo vya maendeleo ya soka katika maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam na Tanga.
Alisema pia kikao hicho kimeridhia kuwapa mikataba mipya ya ajira kwa watendaji wake akiwamo Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, Mkurugenzi wa Ufundi, Oscar Mirambo na Mkurugenzi wa Mashindano, Salum Madadi baada ya kuridhishwa na utendaji wao wa kazi kwa miaka miwili iliyopita.
Kidao alisema anafurahi kuona shirikisho limeendelea kumwamini katika nafasi hiyo na akaahidi ataendelea kutekeleza vema majukumu yake na kulifanya soka la Tanzania kung’ara zaidi kimataifa.