Mchezaji wa zamani wa Simba SC Mtemi Ramadhan ameonyesha kuwahofiwa Wachezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Stephen Aziz Ki kuelekea mchezo wa Ngao wa Jamii, utakaopigwa kesho Jumamosi (Agosti 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC na Young Africans zitakutana kwa mara ya kwanza msimu huu 2022/23, huku mchezo huo ukihitaji mshindi ambaye atatwaa Ngao ya Jamii.
Mtemi ambaye alijitumbukiza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Simba SC miaka miwili iliyopita na baadae kujitoa, amesema Wachezaji hao wawili wanapaswa kuchungwa sana katika mchezo huo, ili wasiharibu siku ya wanasimba ambao wanasubiri ushindi kwa hamu kubwa.
Amesema wawili hao wana uwezo wa kubadilisha matokeo wakati wowote, hivyo amewasihi Wachezaji wa Simba SC kuwa makini muda wote, na kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi linaloongozwa Kocha Zoran Maki.
“Wapinzani wetu wana wachezaji wengi wakuchungwa wakati wote, lakini kwa hawa wawili (Fei Toto na Aziz Ki) ni hatari zaidi, hawa wanaweza kubadili ubao wa matokeo wakati wowote,”
“Wachezaji wa Simba wanapaswa kuwa makini wakati wote, wafuate maelekezo ya Benchi la Ufundi, nina imani wakifanya hivyo tutapata matokeo mazuri kesho.” amesema Mtemi Ramadhan.
Simba SC ina deni la kulipa kisasi cha kufungwa na Young Africans msimu uliopita, wakipoteza mchezo wa Ngao ya Jamii kwa 1-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, pia walikutana na matokeo hayo Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.