MAGWIJI wa Simba SC wamesema kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ atamaliza kesi yake na Young Africans ni mtu sahihi pale Msimbazi msimu ujao; kwani ana nafasi ya kumtoa mtu katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo na akacheza.
Fei Toto yupo kwenye mvutano na mabosi wake juu ya mkataba, ambapo anataka uvunjwe ili aangalie maisha klabu nyingine kutokana na kile anachodai kuwa ni maslahi duni na pia hana furaha ndani ya Young Africans. Klabu hiyo imemshtaki kwenye mamlaka za soka na kuna shauri linaendelea.
Emmanuel Gabriel ‘Batgol’, Henry Joseph na Joseph Kaniki ‘Golota’ waliong’ara Simba SC kwa nyakati tofauti wamesema pamoja na mambo mengine bado umri wake unamruhusu kung’ara lakini Simba SC wasubiri suala la Fei na mabosi wake litamalizika punde.
Batgol aliyejijengea heshima kwa kuinyanyasa Young Africans katika mechi za watani amesema: “Simba SC wakimsajili Fei watakuwa na bahati na wamelamba dume. Pia atawachangamsha Simba SC na ataleta ushindani ndani ya timu, ana nafasi ya kum- toa mtu akacheza.
“Kikubwa amalizane na Young Africans vizuri ili anakoenda awe huru. Namwamini kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambaye anaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye timu.”
Naye Kaniki amesema: “Kwanza Fei umri wake ni mdogo na ana kipaji. Kama watabahatika kumsajili basi litakuwa jambo jema na Fei ana uwezo wa kucheza kwa kocha na timu yoyote, ni suala la mfumo tu.
“Fei yupo kwenye kiwango kizuri na kinapanda. Hizi zingine ni changamoto ambazo wengi wamewahi kuzipitia na maisha yako hivyo.
“Hadi sasa Fei kwa mujibu wa mkataba bado ni mchezaji wa Young Africans na anapaswa kuuheshimu na hata kama ungekuwa unamalizika msimu huu angekuwa ndani ya kiwango bora kisoka, uwezo wake ni mkubwa,” amesema Kaniki ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar.
“Ikumbukwe tu kwamba Simba SC na Young Africans sio mwisho wa maisha ya soka, mpira wa sasa ni sayansi. Wachezaji wanapaswa kuingia mfukoni na kutoa pesa kwa ajili ya kuwa na watu makini wa kuwasimamia kwenye mambo yao kisoka. Suala la Fei tunaombea liishe salama kwani anahitajika sana hata kwenye Taifa.”
Henry ambaye aliwahi kucheza nchini Norway, amesema Fei ni mchezaji mzuri na ana uwezo wa kucheza Simba SC kikosi cha kwanza lakini mabosi wa Wekundu wasitumie nguvu kwenye usajili wa Fei, bali kipindi kama hiki waangalie hata sehemu nyingine kwani kuna wachezaji wazuri.
“Fei anaweza kucheza na kuisaidia Simba SC lakini kwa sasa haina sababu kutumia nguvu kubwa kupata saini yake. Kikubwa ni kumuombea ili tatizo lake na mabosi wake limalizike ndipo wao wamsajili akiwa hana shida na klabu yake,” amesema Henry