Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Felix Sunzu amekiangalia kikosi cha sasa cha timu hiyo na kutamka inahitaji watu wawili ili ifanye vizuri msimu ujao katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa, akiutaka pia kutoacha wachezaji wengi kwa wakati mmoja kwani itawagharamu.
Sunzu, raia wa Zambia alisajiliwa na Simba SC mwaka 2011 akitokea Al Hilal ya Sudan, alikuwa na msimu mzuri kwani mwaka 2011 aliipa timu hiyo taji la ligi, huku akiwa kwenye kikosi kilichoifumua Young Africans mabao 5-0 katika mechi ya kufungia msimu wa 2011-2012 iliyopigwa Mei 6, 2012.
Akizungumza jijini Dar es salaam Sunzu amesema Simba SC haijafanya vibaya msimu uliopita ila inahitaji wachezaji wawili wenye viwango vikubwa ili kuifanya timu iweze kubalance vizuri.
“Simba inahitaji beki wa kati ambaye atasaidiana na Inonga Baka na mshambuliaji mmoja ambaye atasaidiana na Jean Baleke, wasiwaze kuacha watu wengi watakosea sana, wana timu wamekosea sehemu ndogo sana, wajipange tu naamini watafanya vizuri msimu ujao.
“Tatizo la Simba kila siku linajulikana kwenye michuano ya kimataifa ni kushindwa kucheza mipira iliyokufa faulo na kona, hapa wanatakiwa wafanye zaidi mazoezi ili kuliondoa tatizo hilo kwani ni la muda mrefu tangu nikiwa Simba. Nilikuwa narudi nyuma kucheza mipira ya kona, ila bado ilikuwa ni shida na waarabu hiyo ndio mipira yao,” amesema Sunzu anayeichezea kwa sasa Mwanza Veterani.
Kuhusu uwezo wa Wazambia wenzake walipo katika ligi Moses Phiri na Clatous Chama wa Simba na Kennedy Musonda kwa Yanga alisema wanafanya vizuri na anajivunia uwepo wao.
“Wanacheza vizuri sana na wanaipeperusha vyema bendera ya nchi yetu japo Chama anahitaji kusaidiwa kwa sababu hana uwezo wa kukaba ana uwezo wa a kuchezesha timu,” amesema mshambuliaji huyo ambaye ameona mke Mbongo na anaishi Tanzania.