Shirikisho la soka barani Afrika CAF huenda likachukua maamuzi ya kubadilisha muda wa kufanyika kwa fainali za mataifa ya bara hilo (AFCON), ambazo kwa sasa zinafanyika kila baada ya miaka miwili.
CAF wanafikiriwa huenda wakafanya maamuzi hayo, kufuatia ushauri uliotolewa na Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA GianniĀ Infantino, wakati akihutubia kwenye semina ya siku moja, iliyolenga kujadili maendeleo ya soka la Afrika.
Semina hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa shirikisho la soka barani Afrika CAF, nchi wanachama (Mataifa 54 ya Afrika), magwiji wa soka wa Afrika, maafisa kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa, wawekezaji wa makampuni makubwa pamoja na wanahabari, ililenga zaidi kulikuza na kuliendeleza soka la Afrika.
Infantino alichukua nafasi ya kuhutubia kwenye semeina hiyo kwa kuishauri CAF kufanya mabadiliko ya kufanyika kwa fainali za Afrika kufanyika kila baada ya miaka minne, na kuachana na mfumo wa sasa.
Akitolea mfano kauli ya gwiji wa soka duniani Pele ya kusema timu ya Afrika itashinda kombe la dunia, Rais Infantino alisema kushindwa kutimia kwa kauli hiyo ni mambo yanayodhihirisha Afrika haikui kwenye mpira wa miguu, hivyo ni lazima jambo lifanyike kubadili ukurasa huo.
Kiongozi huyo wa soka duniani anaamini kuwa, endapo CAF watakubali ushauri wake wa kubadili mfumo wa kuchezwa fainali za Afrika kila baada ya miaka minne, itaongeza hata hadhi ya kibiashara kwa kile alichosema michuano hiyo kwa sasa inavuna mapato asilimia 20, chini ya kile kinachovunwa kwenye fainali za mataifa ya Ulaya.
Aidha katika semeina hiyo FIFA na CAF wamethibitisha kuwepo kwa makubaliano ya pamoja yaliyojikita kwenye mambo matatu, waamuzi, miundombinu pamoja na mashindano.
Kwa kuanzia FIFA imeamua kuwa na waamuzi bora 20 kutoka barani Afrika, ambao watawapa mikataba ya kudumu na wakiwaendeleza, huku shirikisho hilo likipitisha pendekezo la kugawa dola bilioni moja kwa ajili ya kujenga angalau uwanja moja wa kisasa kwenye kila nchi mwanachama wa CAF.
Hata hivyo FIFA wamethibitisha kwamba kwa nchi ambazo wana viwanja vya namna hiyo, fedha hizo watazipeleka kwenye ujenzi wa miundombinu mingine.