Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa licha ya kumpandisha cheo aliyekuwa msemaji mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas bado ataendelea kuwa Msemaji wa Serikali hadi atakapopatikana mwingine.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 3, 2020 katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam, aliowateua Ijumaa ya wiki iliyopita.

“Tumemteua awe katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kwa sasa hivi ataendelea kuwa Msemaji wa Serikali mpaka tutakapopata mwingine na atakuwa anasema sasa akiwa mkubwa zaidi,” amesema Rais Magufuli na kubainisha kuwa ameamua kumpandisha cheo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya ya kuisemea serikali bila kuchoka.

“Dkt. Abbas amefanya kazi nzuri kama msemaji wa Serikali, hakuchoka aliisemea vizuri Serikali, ningependa aendelee tu kuwa msemaji wa Serikali lakini mahali mtu anapotakiwa kupata promosheni, usimnyime promosheni,” amesema Rais Magufuli.

Viongozi wengine walioapishwa leo ni pamoja na makatibu wa wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Viwanda na Biashara; na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia, Makatibu Tawala wa mikoa mitatu, Tanga,Ruvuma, Mwanza.

Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Brigedia Jenerali Suleiman Mzee aliyechukua nafasi ya aliyekua kamishna Jenerali wa Magereza, Faustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa balozi.

Rais Magufuli pia amemuapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji aliyechukua nafasi ya Thobias Andengenye ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wanajeshi 10 wa Tanzania wafariki kwenye mazoezi, miili yao yachunguzwa
FIFA kuimwagia fedha Afrika, yashauri mfumo wa AFCON ubadilishwe