Mkuu wa wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema wanajeshi kumi wa Jeshi la Wananchi wamefariki dunia wakiwa kwenye mazoezi ya kawaida katika eneo la Msata.

Akizungumza leo, Februari 3, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha viongozi wapya aliowateua wakiwemo Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali, viongozi wa majeshi na viongozi wa Mahakama, Jenerali Mabeyo amesema kuwa askari hao walifariki katika mazoezi ya kawaida ya kukimbia, Januari 30, 2020.

Alisema kuwa baada ya mazoezi ya saa mbili, hali zao zilibadilika na wakakimbizwa katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo ambapo kumi walifariki dunia na wengine hali zao ziliimarika.

“Tunahisi walikula chakula chenye sumu, labda wakati wanatembea walinunua vyakula barabarani vikawadhuru; mazoezi yalikuwa ya kawaida tu,” alisema Jenerali Mabeyo.

Aliongeza kuwa sampuli ya miili ya marehemu imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kubaini chanzo cha vifo hivyo.

Mkuu huyo wa Majeshi alisema kuwa hadi sasa kuna majeruhi watano kutokana na tukio hilo.

Mbowe amuandikia barua Magufuli kufuta matokeo ya uchaguzi Serikali za mitaa
Magufuli: Dkt. Abbas ataendelea kuwa Msemaji wa Serikali akiwa mkubwa zaidi