Shirikisho la Soka la duniani FIFA limependekeza kanuni ya mabadiliko ya wachezaji mpaka watano kwenye mchezo mmoja, kutokana na ratiba ngumu zitakazozikabili timu mara ligi mbalimbali zitakaporejea.
FIFA wamependekeza kanuni hiyo, na kueleza itatumika kwa muda endapo itaafikiwa na kupitishwa na chombo husika.
Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka ‘International Football Association Board’ (IFAB) pamoja na chombo cha kusimamia kanuni za soka (football’s rule-making body), imeachiwa jukumu la kujadili na kupitisha pendekezo hilo na baadae kuliwasilisha kwenye vyama vya soka duniani kote.
Kuhusu ni lini ligi zitarejea, Msemaji wa FIFA amesema soka litatakiwa kurejea kipindi ambacho mamlaka za afya katika serikali husika zitajiridhisha kuhusu usalama wa afya za watu wake na kuthibisha kuwa ligi haitaathiri huduma na mwenendo wa afya kwa wananchi.