Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Fiston Kalala Mayele amesema yeye na wachezaji wenzake hawana ‘Presha’ kuhusu mchezo wa raundi ya pili ya mtoano dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Mayele ametoa kauli hiyo kwa kujiamini akisema ni halali yao kuingia makundi katika michuano ya Kombe la Mabingwa Afrika kwani wana wachezaji wazuri na wanajiamini, hivyo hawana Presha.
“Kuhusu mchezo dhidi ya Al Hilal, wachezaji hatuna presha kabisa. Young Africans tuna wachezaji wakubwa waliozoea michezo yenye Presha kama Bangala, Djuma, Morrison, Aziz Ki na wengine, tumezioe presha.”
“Mfano mimi mechi yangu kubwa ya kwanza ya kimataifa CAF nikiwa AS Vita nilicheza dhidi ya Kabylie ya Algeria na Raja Casablanca ya Morocco, ule uwanja ulijaa kabisa, kwa hiyo tumezoea ile Presha.”
“Kwa hiyo tutajitahidi hapa kwetu tupate matokeo mazuri, na kule kwao tutakwenda kupambana tena ili tuingine makundi,” amesema Mayele.
Ikumbukwe kuwa Young Africans wametinga raundi ya pili ya mtoano baada ya kuitoa Zalan FC kwa jumla ya bao 9-0, ambapo hatua inayofuata watakutana na Al Hilal ambayo inafundishwa na aliyekuwa kocha wa AS Vita na RS Berkane, Frolent Ibenge raia wa Congo DR.