Mshambuliaji wa kutumainiwa Young Africans Fiston Kalala Mayele ameeleza namna wachezaji kambini wanavyotamani kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger.

Young Africans imetinga Fainali ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni mara ya kwanza kufikia hapo kwenye michuano ya Afrika.

Mayele ambaye ni raia wa DR Congo amesema kila mchezaji kambini anasubiri kwa hamu timu hiyo kutwaa ubingwa mwezi ujao na kila hatua wanazungumzia hilo.

Staa huyo anaongoza kwa kufunga mabao kwenye Kombe la Shirikisho akiwa ameshafunga sita na pia anaongoza kwenye Ligi Kuu Bara alikofunga mabao 16 zikiwa zimebaki mechi mbili ligi imalizike.

“Akili zetu zote zipo katika mchezo muhimu unaowakilisha Taifa na nguvu zetu tumeweka huko ili kuhakikisha tunafanya vizuri. Kambini kwetu kwa sasa kila mmoja anatamani kutwaa ubingwa na hayo ndiyo mazungumzo ambayo yamekuwa yakitawala,” amesema Mayele.

“Lakini wakati mwingine tunapeana mbinu za hapa na pale kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo wa fainali, kila mmoja amekuwa akimhimiza mwenzake kuhakikisha anafanya vizuri. Fainali yoyote siyo ya kupuuzwa kwetu ndio maana tunafanya maandalizi makubwa ili kufanya vizuri na kurudisha heshima kikosini kwetu.”

Young Africans inatakiwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani Jumapili kabla haijaenda kumaliza kazi Algeria Juni 3.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Young Africans kukutana na USM Alger kwani iliwahi kuvaana nayo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Barani Shirikisho, Mei 2018 huko Algers, Algeria ilikofungwa mabao 4-0 kisha ikalipa kisasi kwa Mkapa kwa mabao 2-1.

Chino arudisha majibu kwa Ibrahim Class
Azam FC yaipotezea Young Africans ASFC