Miamba ya soka nchini Saudi Arabia ina mpango wa kuibomoa Young Africans baada kuweka ofa mezani ya kuhitaji saini ya mshambuliaji wao kinara, Fiston Kalala Mayele.
Mayele ambaye msimu huu amekuwa na mafanikio makubwa katika timu hiyo akifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kufunga mabao saba huku akisaidia timu yake kucheza fainali ya michuano hiyo ambayo ilishindwa kuutwaa ubingwa mbele ya USM Alger.
Msimu huu katika Ligi Kuu Bara mshambuliaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 17 na kuiwezesha Young Africans kutetea ubingwa huo.
Taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na mshambuliaji huyo zinasema kuwa Mayele amepokea ofa nyingi za kutoka nje ya mipaka ya Tanzania ikiwemo AL Qadisiyah, kwa nia ya kutaka saini yake kuelekea katika msimu ujao wa ligi Chanzo hicho kilisema kwamba, Klabu ya Al Qadisiyah ambayo anacheza Simon Msuva na Walter Bwalya, wamepewa taarifa zake.
“Nadhani kila mtu anajua kwamba Mayele kubakia Young Africans anga msimu ujao ni jambo gumu kutokana na mafanikio ambayo ameyapata msimu huu na ukiangalia aliyempeleka Msuva kule Saudi Arabia ndiyo anayemsimamia Mayele,” amesema mtoa taarifa hizi
Alipotafutwa Mayele kuhusu suala hilo amesema: “Siwezi kusema jambo lolote juu ya hatima yangu ya kubakia Yanga kwa sasa hadi msimu utakapokuwa umemalizika, nataka kuweka nguvu yangu kwenye mechi zilizobaki ligi na fainali ya Kombe la FA na baada ya hapo ndiyo naweza kujua kama nitaondoka au nitabakia Young Africans.
Rais wa Young Africans, Injia Hersi Said tayari alishaweka wazi juu ya mchezaji yoyote kama atatakiwa na timu nyingine wampe machaguo matatu ikiwemo kumboreshea maslahi ya mkataba wake huku akisisitiza hawatokuwa tayari kuzuia mchezaji yeyote ambaye atakuwa amepokea masilahi mazuri.