Wakati Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu wa 2021/22 ikielekea ukingoni, Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele anahusishwa na mpango wa kuachana na klabu hiyo, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kisoka na kuzifumania nyavu za timu pinzani.
Mayele ambaye amefunga zaidi ya mabao 10 katika ligi hiyo, anahusishwa na mpango wa kuwaniwa na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane, chini ya Kocha Mkuu Florent Ibenge.
Kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali vya habari kutoka Congo DR vimethibitisha kuwa, Kocha Ibenge ambaye aliwahi kufanya kazi na Mayele katika klabu ya AS Vita, amevutiwa na uwezo wa Mshambuliaji huyo baada ya kumfuatilia kwa ukaribu akiwa Young Africans msimu huu 2021/22.
Hata hivyo Uongozi wa Young Africans umesema bado haujapata taarifa zozote kuhusu mpango huo wa RS Berkane, na kama itathibitika uwepo wa ofa hiyo, watawafahamisha Mashabiki na Wanachama wao kupitia vyanzo vyao vya habari.
Kama Ibenge atafanikisha kumsajili Mayele, itakua mara ya pili mfululizo kufanya hivyo kwani msimu uliopita alimsaili Kiungo Mshambuliaji Tuisila Kisinda ambaye aliwika akiwa na Young Africans msimu wa 2020/21.
Pia alimsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka Zambia na Simba SC Clatous Chama, baada ya kuvutiwa na uwezo wake, lakini Kiungo huyo alirejea Tanzania wakati wa Dirisha Dogo la Usajili kwa kigezo cha changamoto ya mazingira ya kimaisha na Soka la Morocco.