Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele ameahidi kuanza msimu mpya wa 2022/23 kwa aina tofauti ya Ushangiliaji.
Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo aliteka Soka la Bongo msimu uliopita 2021/22, kwa aina ya kushangilia kwa KUTETEMA, ambayo ilizungumzwa kila kona ya nchi.
Mshambuliaji huyo ambaye yupo njiani kurejea Dar es salaam, amesema amejipanga kuja na aina mpya ya Ushangiliaji, ambayo ana uhakika itakua nzuri zaidi ya KUTETEMA.
Amesema ametafakari na kubaini kuja na kitu tofauti, ambacho kitaendelea kuwafurahisha Mashabiki wa Young Africans, ambao amedai siku zote walimpa ushirikiano tangu aliposajiliwa klabuni hapo mwanzoni mwa msimu uliopita, akitoka AS Vita ya nchini kwao DR Congo.
“Msimu ujao sitatetema tena kama ambavyo nilikua nikifanya katika msimu uliomalizika hivi karibuni nitakuja na aina mpya ya kushangilia ambayo hakuna mtu ambaye amewahi kuiona.”
“Nategemea aina hiyo mpya wa kushangilia nitaizidua siku ya gao ya Jamii, hii ni kutokana na hata ile ya msimu uliopita (KUTETEMA) niliizindua katika mchezo dhidi ya Simba SC.” Amesema Mshambuliaji huyo.
Mayele alimaliza msimu wa 2021/22 akifunga mabao 16 kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akitanguliwa na Mshambuliaji mzawa George Mpole wa Geita Gold FC aliyefunga mabao 17.