Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele, amewaahidi makubwa Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, baada ya kuanza vizuri Msimu wa 2022/23.
Young Africans ilianza kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania iliyokua nyumbani Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha siku ya Jumanne (Agosti 16).
Mayele ambaye alifunga bao la kusawazisha kwenye mchezo huo amesema hatua ya kuanza vizuri katika Uwanja wa ugenini ni njema kwa Young Africans na inaonyesha msimu huu utaendelea kuwa wa furaha kwao.
Amesema kuanza vyema ugenini kwa kupata ushindi uliowapa alama tatu ni jambo kubwa huku akiendelea kufunga, hivyo anaona ni kama wanaendeleza pale walipoishia msimu uliopita.
“Kupata alama tatu ugenini ni jambo zuri, nimeanza kwa kufunga bao langu la kwanza msimu huu katika Ligi, sasa tunaendelea tulipoishia, tunawahakikishia Mashabiki mambo mazuri yanakuja zaidi ya walioyapata msimu uliopita.” Amesema Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo
Mchezo wa Mzunguuko wa Pili Young Africans itaendelea kuwa Ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kwa kucheza dhidi ya wenyeji wao Coastal Union kutoka Tanga.
Wawili hao kwa mara ya mwisho walikutana Uwanjani hapo katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na kuambulia matokeo ya sare ya 3-3, kabla ya sheria ya Matuta kuchukua mkondo wake na kuibeba Young Africans.