Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda amesema anaiheshimu sana Young Africans kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/23.

Coastal Union kesho Jumamosi (Agosti 20) itakua mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, huku ikichagizwa na matokeo ya 1-0 dhidi ya KMC FC.

Kocha Mgunda amesema Young Africans ina sifa kubwa sana katika nchi ya Tanzania na imesheheni wachezaji wazuri na Benchi la Ufundi zuri, hivyo hana budi kuipa heshima yake kuelekea kesho Jumamosi.

Amesema heshima anayoipa Klabu hiyo ya Jangwani-Dar es salaam haimaanishi kama anaihofia, bali anafanya hivyo kwa kutimiza wajibu wa mchezo wa soka, ambao unatoa nafasi kwa mtu yoyote kumuheshimu mpinzani wake kwanza.

“Haimaanishi kama ninaihofia Young Africans, nipo tayari kupambana nayo kesho Jumamosi, nilichokisema hapa ni kuiheshimu kwa sababu mchezo wa soka unatutaka tuwaheshimu wapinzani wetu, ima awe mkubwa ama mdogo.”

“Nafahamu walicheza hapa Sheikh Amri Abied na wakashinda dhidi ya Polisi Tanzania, nimebahatika kuwaona na kujiridhisha ubora wao japo kuna udhaifu niliouona na nitautumia kwenye mchezo wa kesho Jumamosi ili tuweze kupata matokeo mazuri.”

“Mbali na kuwasoma na kutambua wapi wana udhaifu, hata kwa upande wetu tumejiandaa kurekebisha makosa yetu ambayo yalionekana katika mchezo wa kwanza dhidi ya KMC FC, kwa hiyo kesho tutaingia tukiwa kamili kwa kupambana na Young Africans.” amesema Mgunda

Wawili hao kwa mara ya mwisho walikutana Uwanjani hapo katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na kuambulia matokeo ya sare ya 3-3, kabla ya sheria ya Matuta kuchukua mkondo wake na kuibeba Young Africans.

Kocha Coastal Union afunguka mazito aliyopitia
Fiston Mayele: Tutachukua tena msimu huu