Mshambualiji kutoka nchini Burundi Fiston Abdul-Razaq amechukizwa na maamuzi ya Uongozi wa Young Africans ya kumuachia kirahisi Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Tuisila Kisinda.
Young Africans imeafiki kumuuza Tuisila Kisinda kwenye klabu ya RS Berkane ya Morocco, katika kipindi hiki cha dirisha la usajili, kufuatia shinikizo la kocha wake za zamani Florent Ibenge.
Ibenge amekabidhiwa benchi la ufundi la klabu hiyo akitokea AS Vita Club ya DR Congo, na ameanza kupanga kikosi chake bora kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Morocco.
Fiston ambaye amemaliza mkataba wake na Young Africans tangu mwishoni mwa msimu wa 2020/21, amesema Uongozi wa klabu hiyo umefanya makosa makubwa sana kukubali kumuachia Tuisila.
Amesema kiungo huyo alikua na umuhimu mkubwa sana kwenye kikosi cha Young Africans, na msimu ujao ulikua sahihi kuendelea kuwa sehemu ya klabu hiyo, inayosaka ubingwa wa Tanzania Bara kwa zaidi ya misimu mitatu.
“Sawa tumeondoka Young Africans lakini Tuisila uongozi ungejitahidi kumbakiza, alikuwa muhimu sana katika kupeleka mashambulizi, na ikizingatia Young Africans sasa hivi inajijenga zaidi kuwa na kombinesheni nzuri,”
“Sawa kwenda timu nyingine sio mbaya kwa kuwa mpira ndio kazi yake, lakini sio wakati huu, kwanza alianza kuijua na kuisoma Ligi ya Tanzania,” amesema Fiston ambaye bado yupo nchini licha ya kuachana na Young Africans.