Kocha mkuu wa klabu ya RS Berkane ya nchini Morroco, Florent Ibenge amesema kuwa klabu ya Simba imepata moja kati ya makocha wakubwa ambao wamepata uzoefu katika timu kubwa jambo ambalo anaamini litaisaidia timu hiyo kufanya vizuri.
Ibenge aliwahi kuhusishwa kujiunga na Simba kabla ya timu hiyo kumshusha Didier Gomes msimu uliopita wakati kocha huyo akiwa anaifundisha klabu ya AS Vita ya nchini DR Congo.
Uongozi wa Simba mwishoni mwa juma lililopita ulimtangaza kocha wake mpya Pablo Franco, mwenye uraia wa Hispania ambapo kocha huyo amewahi kufundisha katika timu za Real Madrid na Getafe za nchini Hispania.
Ibenge alisema kuwa Simba imepata moja kati ya makocha wakubwa wenye uzoefu wa kufundisha katika vilabu vikubwa jambo ambalo anaamini litaifanya timu hiyo kupata mafanikio makubwa chini ya kocha huyo.
“Simba imepata kocha mkubwa ambaye naamini ataenda kuwapa mafaniko makubwa, ni nadra sana katika ukanda kama ambao Simba ipo kuona kocha mkubwa kama yeye, ni bahati sana kwao lakini hayo ni maendeleo ya soka yanajidhihirisha.
“Siku zote mpira ili timu ipate mafanikio lazima ifanye mambo makubwa, iwe na kocha mwenye uwezo mkubwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa hapo lazima timu iweze kushinda vikombe vikubwa, naiona Simba ikiwa katika kutekeleza hayo,”alisema kocha huyo.