Bunge la Jimbo la Florida nchini Marekani limepitisha muswada wa usalama shuleni ambao unaweka marufuku mpya ya uuzaji wa bunduki na kutoa mafunzo kwa baadhi ya walimu kumiliki silaha.
Baada ya kupitishwa kwa muswada huo sasa unapelekwa kwa gavana ili kutiwa saini.
Muswada huo uliungwa mkono kwa kura 67 dhidi ya 50 ukiwa mchanganyiko wa wabunge wa Chama cha Republican waliounga mkono dhidi ya Democrats walioupinga.
Muswada huu wa sheria unaoungwa mkono na familia za waathirika ni matokeo ya shambulio lililotokea katika Shule ya Sekondari ya Parkland na kusababisha mauaji ya watu 17.
Andrew Pollack, ambaye alimpoteza binti yake, Meadow mwenye umri wa miaka 18 katika shambulio lililofanyika katika shule ya Sekondari ya Marjory Stoneman Douglas na Ryan Petty, ambaye alimpoteza binti yake Alaina mwenye umri wa miaka 14 wamesema muswada huo una mambo mazuri na unastahili kupitishwa.
Muswada huo utaweka umri wa chini wa kununua bunduki kuwa kati ya miaka 18 na 21 na kuweka kipindi cha matazamio kuhusu uuzaji wa silaha.
Pia utaweka programu ya mwongozo ambayo itawezesha waajiriwa wa shule na walimu wengi kubeba silaha za mkononi endapo watapatiwa mafunzo ya ulinzi na endapo utawala wa shule utaamua kushiriki katika programu hiyo.
Mambo mengine yatakayoundwa ni kuanzisha programu za afya ya akili katika shule, kuanzisha namba ya mawasiliano ya simu ambayo itatumika kutoa taarifa bila ya mtoa taarifa kujitambulisha ambayo itatumika kwa wanafunzi na watu wengine kuripoti vitisho katika shule na kuimarisha mawasiliano kati ya shule, vyombo vya ulinzi na taasisi za serikali.