Aliyekuwa Kiungo wa klabu ya Simba Gerson Fraga Vieira amefanyiwa upasuaji wa goti nchini kwao Brazil, baada ya kuumia akiwa kwenye majukumu ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita.
Fraga aliumia goti akiwa kwenye mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC dhidi ya Biashara United waliokubali kufungwa mabao manne kwa sifuri Septemba, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kiungo huyo alilazimika kurejea nyumbani kwao Brazil, baada ya kusitishiwa mkataba wake na uongozi wa Simba SC, na aliendelea na matibabu ya awali kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Kuondoka kwa kiungo huyo, kunaifanya Simba kuwa na nafasi moja ya usajili wa mchezaji wa kimataifa, na huenda akasajiliwa hivi karibuni kwa ajili ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Fraga alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Atlético de Kolkata ya India, na alikua sehemu ya kikosi kilichoisaidia klabu hiyo ya Msimbazi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho msimu wa 2019/20.