Chama cha waamuzi wa soka nchini Tanzania (FRAT) kimetoa kauli ya pongezi baada ya shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kumteua mwamuzi Frank John Komba kuwa miongoni mwa watakaochezesha fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika nchini Gabon mwezi ujao.
Mwenyekiti wa FRAT, Mohamed Nassoro amesema kuteuliwa kwa mwamuzi Komba katika orodha ya waamuzi wasaidizi kwa ajili ya fainali hizo za vijana, ni hatua kubwa kwa Tanzania ambayo miaka kadhaa ilikua haipati nafasi hiyo.
Mohamed Nassoro amesema hatua hiyo inawezesha waamuzi wengine kuendelea kufanya kazi zao kwa kujiamini, huku wakijua kuna nafasi adhimu kama aliyoipata Komba katika fainali za vijana za Afrika.
“Komba ni mwamuzi mwenye nidhamu, na ninataka kukuhakikishia atafanya vizuri katika utendaji wake wa kazi akiwa nchini Gabon,”
“Naamini kijana huyu alipata malezi mazuri tangu akiwa mdogo, hii imekua siri kubwa ya mafanikio yake hadi kufikia hatua ya CAF kumuona na kumteua kuwa miongoni mwa waamuzi wa akiba watakaokwenda Gabon, kwa kweli nimefarijika sana na uteuzi wake,” amesema Mohamed Nassoro
Wakati huo huo Mohamed Nassoro wamewataka waamuzi watakaopewa jukumu la kuchezesha michezo ya lala salama ya ligi kuu ya soka Tanzania bara kufanya kazi zao kwa uweledi ili kutimiza wajibu wa kutoa haki.
Amesema anatambua waamuzi watakaopata nafasi hiyo wana uwezo wa kuchezesha kwa kuzingatia sheria 17 za mchezo wa soka, hivyo halitokua jambo la busara kwa yoyote kuharibu kazi yake kwa kuwanufaisha wachache.