Wanawake wameaswa kujikita kwenye fani mbali mbali za Teknolojia na kuingia kwenye uongozi kwani hakuna jambo ambalo haliwezekani kufanyika na mwanamke.
Akizungumza na Dar24Media katika mdahalo wa masuala ya Sayansi na Teknolojia kwa wanawake, Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Anna Ngoo, amesema mdahalo huo utawasaidia wanawake vijana kuweza kujikita katika masuala ya Teknolojia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Teknolojia itarahisisha mambo mengi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija, kwa sababu hivi sasa teknolojia imekuwa kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia kuhusu uchumi na Teknolojia, Iku Mwanjisi kutoka Jukwaa Maalumu kwa ajili ya wanawake wenye mawazo ya kibunifu na ujasiliamali (Ndoto HUB), amesema katika kukuza uchumi au kuleta maendeleo, lazima mwanamke ashirikishwe.
Patience Abraham kutoka kumbi ya Ubunifu ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Buni innovation Hub), amesema dhumuni la mdahalo ni kuwahamasisha wanawake kujihusisha na masuala ya teknolojia.
“Katika mdahalo huu, kutakuwa na wadau kutoka sekta mbali mbali wakiwemo Vodacom, UNDP na Women in Technology ambapo kwa pamoja watajadili na kuhamasisha wanawake kujitambua katika masuala teknolojia na ubunifu,” Amesema Patience.
Mmoja wa wanufaika wa tamasha hilo, Subira Hamisi ambae ni mwanafunzi wa Chuo Cha Ustawi wa Jamii amesema, lengo la kuwepo katika tamasha hilo ni kujifunza na kujua mambo tofauti kuhusiana na mwanamke, jinsi ya kuwezeshwa na pia anatarajia kujifunza zaidi namna ya kutumia teknolojia.