Beki wa kushoto wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Gadiel Michael, ameendelea kupambana na wadau wa soka wanaomshambulia kupitia mitandao ya kijamii, kuhusu kukaa kwake Benchi na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu hao wa Msimbazi.
Gadiel amekua na wakati mgumu wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC tangu aliposajili msimu wa 2019/20, akitokea Young Africans, ambayo aliihama kufuatia mkataba wake kufikia kikomo.
Beki huyo ambaye aliwahi kutamba na klabu za Azam FC na Young Africans sanjari na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, kwa kueleza kuwa, anaamini muda wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC haujafika na ukifika atatumikia kama livyo kwa wachezaji wengine.
“Mpira ni mchezo wa Nafasi kila Mchezaji anatamani kucheza hivyo Wakati mwingine Nafasi inatakiwa uvumilie na uitafte ipatikane Mimi nafanya hivyo Wakati ukifika wanao penda kuniona nikicheza wataniona.” ameandika Gadiel
Beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye pia ni nahodha msaidizi wa Simba SC amekua chaguo la kwanza la makocha waliopita kwenye klabu hiyo, huku Gadiel Michael akiendelea kukaa Benchi, jambo ambalo limekua likitoa msukumo kwa wadau wa soka kumshawishi aondoke Msimbazi na kusaka klabu ya kuitumikia.