Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Angel Gamondi amedhamiria kupata ushindi wa kwanza katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kusitisha mapumziko ya wachezaji na kuanza maandalizi ya kuelekea mchezo wao wa kesho Ijumaa (Desemba 08) dhidi ya Medeama FC.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 4 usiku na kocha huyo raia wa Argentina amepanga kuutumia mchezo huo kupata ushindi wa kwanza kwa timu hiyo kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mwaka 1998 Young Africans iliposhiriki kwa mara ya kwanza hatua hiyo ilipangwa kundi moja na timu za Raja Casablanca ya Morocco, Manning Rangers ya Afrika Kusini na Asec Mimosas ya Ivory Coast na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Manning Rangers.
Akizungumzia programu za timu hiyo kwa niaba ya Kocha Mkuu, Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison amesema mkuu huyo wa benchi la ufundi alisitisha mapumziko kwa wachezaji baada ya kikosi hicho kuwasili Mji wa Kumasi nchini Ghana ambako ndipo mechi hiyo itakapochezwa.
“Kocha amedhamiria kupata ushindi katika mchezo wetu wa kesho maana alisitisha mapumziko kwa wachezaji baada ya kufika tukafanya mazoezi ya kuondoa uchovu wa safari na jana asubuhi tulifanya mazoezi ya Gym na jioni funatarajia kufanya mazoezi ya uwanjani tutafanya hivyo leo katika uwanja utakaotumika kwa mchezo husika,” amesema Walter.
Kiongozi huyo amesema wachezaji wao wote wapo katika hali nzuri na wamepania kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kurudisha matumaini ya kufuzu hatua ya Robo Fainali kama ambavyo wamekusudia baada ya kuingia makundi.
Meneja huyo amesema safari yao kutoka Dar es salaam hadi wanafika Kumasi ilikuwa shwari hawajakutana na changamoto zozote wakiwa njiani na hata baada ya kuwasili Ghana kitu ambacho kinawapa ari yakufanya vizuri kwenye mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa.
Naye Daktari wa timu hiyo, Moses Etutu amesema wachezaji wote waliosafiri na timu hiyo wapo katika hali nzuri na hakuna mchezaji mwenye changamoto yoyote itakayosababisha kukosa mchezo huo.