Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Angel Gamondi amewataka wachezaji wake kucheza kwa kufuata maelekezo na mbinu alizowapa mazoezini katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mabingwa watetezi Al Ahly.

Young Africans imedhamiria kushinda mchezo huo ambao utachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (Desemba 02) hii kuanzia saa 4:00 usiku.

Kocha huyo amesema lengo lake ni kutaka wachezaji wake kuwaheshimu wapinzani wao kulingana na uzoefu na ubora waliokuwa nao katika mashindano hayo.

“Hatupaswi kucheza kwa kukamia sababu huenda tukashindwa kutimiza kwa ufanisi kile tulichoelekezana mazoezini, lakini Al Ahly ni timu kubwa tuna takiwa kucheza kimbinu zaidi ili kupata tunachokitaka,” amesema Gamondi.

Kocha huyo amesema anaimani kubwa na wachezaji wake kutokana na uzoefu waliokuwa nao katika mechi kama hiyo, hivyo anaamini hawatamwangusha.

Akizungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo huo, Gamondi amesema wamejipanga kuishangaza Afrika kwa kupata ushindi wa kwanza katika hatua hiyo ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Amesema baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya CR Belouizdad wamebaini makosa yao na wanaendelea kuyafanyia marekebisho lengo ni kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wa nyumbani kuchukua pointi zote tisa katika mechi tatu watakazocheza nyumbani.

Young Africans imejichimbia kambini Avic Town, Kigamboni kujiandaa na mchezo huo ambao umepewa jina la Ibrahim Bacca Day.

Ajali ni Ugonjwa usioambukiza - RSA
Ajali ya Basi kugonga Treni yauwa 13 Manyoni