Meneja wa klabu ya Real Madrid, Julen Lopetegui amesema mshambuliaji kutoka nchini Wales, Gareth Bale ana viwango vya kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Cristiano Ronaldo, aliyetimkia kwa mabingwa wa soka Italia Juventus FC.
Lopetegui amezungumzia matarajio ya mshambuliaji huyo akiwa nchini Marekani, ambapo kikosi chake kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya, na usiku wa kuamkia leo kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Man Utd na kukubali kulamba shubiri kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.
Meneja huyo aliyechukua nafasi ya Zidane mwezi Juni, amesema mpaka sasa ana uhakika Bale ana kila sababu ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Ronaldo, kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa mazoezini.
“Cristiano Ronaldo alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi hiki, lakini kuondoka kwake kumetoa nafasi kwa mtu mwingine kuonesha uwezo wa kupambana na huenda akaziba pengo lililowazi, na huyo si mwingine ni Gareth Bale,” alisema Lopetegui.
“Tangu alipojiunga na kambi mwezi uliopita amekua na uwezo mkubwa katika mazoezi, na ninaamini anaweza kufanikisha mambo makubwa ziadi tutakapoanza ligi kuu ya Hispania na harakati za kutetea taji la Ulaya msimu ujao,”
“Sitaki kuwa mnafiki katika hilo, Bale ana kila sababu ya kuwa mrithi wa Ronaldo na mpaka sasa ninatafakari kama nitaweza kuongeza mchezaji mwingine katika safu ya ushambuliaji, baada ya kuona ninachokiona tukiwa hapa Marekani.”
Bale alikua na wakati mgumu wa kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza wakati wa utawala wa meneja Zinedine Zidane, na badala yake alitumika kama mchezaji wa akiba mara kwa mara.
Ronaldo aliihama Real Madrid mwezi uliopita kwa ada ya Euro milioni 100 sawa na dola za kimarekani milioni 117.37.
Real Madrid wanatarajia kuanza msimu kwa kucheza mchezo wa kuwania ubingwa wa UEFA Super Cup dhidi ya mabingwa wa michuano ya Europa League Atletico Madrid, Agusti 15.
Upande wa ligi ya Hispania wataanza kukutana na Getafe August 19.