Aliyekua mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la soka nchini Croatia, Romeo Jozak ametangazwa kushika wadhifa wa ukuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Kuwait.

Jozak ambaye aliwahi kuwa meneja wa klabu ya Legia Warsaw ya nchini Poland, amethibitisha taarifa za kuajiriwa huko Kuwait kama kocha mkuu, kupitia mitandao ya kijamii.

Jozak amesaini mkataba wa miaka miwili na kazi kubwa inayomkabili ni kuiwezesha timu ya taifa ya Kuwait kufanya vizuri katika medani ya soka, baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa kwa miaka miwili iliyotolewa na shirikisho la soka duniani FIFA.

Kuwait ilifungiwa kujihusisha na soka, kufuatia masuala ya kisiasa nchini humo, ambayo yaliingilia mamlaka za soka, jambo ambalo lilikwenda kinyume na kanuni na taratibu za mpira wa miguu duniani.

Hata hivyo tayari Kuwait imeshatangaza kutoshiriki fainali za mataifa ya barani Asia ambazo zitaunguruma mwanzoni mwa mwaka 2019 Falme Za Kiarabu, huku viongozi wa shirikisho la soka nchini humo wakiweka mipango ya kuanza mchakato wa kuwania kucheza michuano ya Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo-Japan.

Jozak, mwenye umri wa miaka 45, alifanya kazi na shirikisho la soka nchini Croatia hadi mwezi Machi mwaka 2017, na baadae aliajiriwa na klabu ya Legia Warsaw kama meneja/kocha, kabla ya kutimuliwa mwezi April mwaka huu 2018.

Serikali yawabana wachungaji, yataka makanisa kutozwa ushuru
Mahakama yalitoa MwanaHalisi kifungoni, lakutana na kiunzi kingine