Uongozi wa klabu ya Everton unajipanga kumsainisha mkataba mpya mlinda mlango Jordan Pickford, ili kuzima harakati za klabu ya Chelsea ambayo inatajwa kuwa kwenye mikakati ya kutuma ofa ya kumsajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mapema mwezi ujao.

Pickford, amekua lulu nchini England baada ya kuonyesha umahiri katika lango la timu ya taifa la nchi hiyo, wakati wa fainali za kombe la dunia zilizomalizika nchini Urusi Julai 15.

Chelsea wanatajwa kuwa katika harakati za kutuma ofa ya kumsajili mlinda mlango huyo ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Sunderland, kufuatia changamoto inayowakabili kwa sasa ya kutokua na uhakika wa kuendelea kumtumia Thibaut Courtois, baada ya kugoma kusaini mkataba mpya.

Mkataba wa Courtois, utafikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2018/19, na tayari anahusishwa na mipango ya kujiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid

Uongozi wa Chelsea unaamini kama utafanikiwa kumpata Pickford, utakua umelamba dume, kutokana na kiwango cha mlinda mlango huyo kuendenana na hadhi ya ushindani mkubwa katika ligi ya England pamoja na nje ya nchi hiyo, hususan kwenye ushiriki wao kimataifa msimu ujao.

Mapema hii leo, gazeti la The Sun limechapisha habari iliyoeleza kuwa, uongozi wa Everton umejipanga kumsainisha mkataba mnono mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 24, kama sehemu ya kutoa msisitizo wa kuendelea kumuhitaji klabuni hapo.

Mkataba mpya kwa Pickford utakua wa mapema mno, baada ya kusajiliwa msimu uliopita na kusainishwa mkataba wa miaka mitano uliokua na gharama ya Pauni milioni 30.

Katika hatua nyingine gazeti la The Sun limetanabaisha kuwa, endapo Chelsea watashindwa kukamilisha mpango wa kumsajili Pickford, itawalazimu kuuwahi muda wa dirisha la usajili kabla halijafungwa kwa kumsajili mlinda mlango wa klabu ya Stoke City Jack Butland.

Inaamiwa wazi Batland atakua tayari kusajiliwa na klabu hiyo, kufuatia hitaji lake la kutaka kucheza ligi kuu, baada ya Stoke City kushuka daraja msimu uliopita.

JPM awakaribisha mabalozi jijini Dodoma
Zao la Mchikichi latangazwa kuwa la Kibiashara