Kiungo kutoka nchini Ghana Michael Kojo Essien ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa (Black Stars), na kusema ni zamu wa vijana kulisaidia taifa hilo la Afrika Magharibi katika medani ya soka la kimataifa.

Kiungo huyo wa zamani wa klabu ya Chelsea ya England, ametangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa, baada ya kuitumikia timu hiyo kwa kipindi cha miaka 12.

Kwa mara ya mwisho alijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ghana, wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2014, zilizochezwa nchini Brazil.

Anakua mchezaji wa tatu kutangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa miongoni mwa wachezaji walioitwa wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2014, akitanguliwa na Sulley Muntari na Kevin-Prince Boateng, ambao walifunkuzwa kambini kutokana na sababu za utovu wa nidhamu.

“Nimefanya maamuzi ya kuachana na timu ya taifa, nimetafakari kwa kina na nimeona kuna ulazima wa kufanya hivyo,” Alisema Essien alipokua akihojiwa na GHOne TV.

“Kama unakumbuka, niliwahi kutangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa kabla ya fainali za kombe la dunia mwaka 2014, lakini kocha [Kwesi Appiah] aliniita kikosini na nilikubali wito, kwa sasa ninaona muda wa kufanya hivyo kikamilifu umewadia.

“Ghana ina wachezaji wengi vijana ambao wana uwezo mkubwa wa kucheza katika timu ya taifa, ninaamini watakua na kila sababu ya kufika mbali zaidi ya tulipofika sisi, wanahitaji kupewa nafasi na kuthaminiwa katika mapambano ya taifa lao.” Aliongeza Essien.

Essien alianza kuitumikia timu ya taifa ya Ghana mwaka 2002, na mpaka anatangaza kustaafu, ameshacheza michezo 58 na kufunga mabao tisa.

Alikua miongoni mwa wachezaji wakutumainiwa wakati Ghana waliposhiriki kwa mara ya kwanza fainali za kombe la dunia mwaka 2006 zilizofanyika nchini Ujerumani.

Essien mwenye umri wa miaka 35 kwa sasa hana klabu ya kuitumikia baada ya kuachana na klabu ya Persib Bandung ya nchini Indonesia, kufuatia mkataba wa mwaka mmoja aliousaini na uongozi wa klabu hiyo kufikia kikomo mwezi uliopita.

Video: Mnyukano CCM asilia, wahamiaji, Waziri Lugola awekwa njia panda.
Mnangagwa ajipima ubavu kwa Mugabe, ‘ni mimi au Mugabe’