Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amejibu kauli ya aliyekuwa Bosi wake, Robert Mugabe ambaye jana aliweka wazi kuwa hatampigia kura kwenye uchaguzi mkuu unaofanyika leo.

Kupitia kipande cha video kilichowekwa kwenye mtandao wa Twitter kupitia akaunti ya kiongozi mwandamizi wa Zanu-PF, Nick Mangwana, Rais huyo wa Zimbabwe amesema kuwa ni dhahiri sasa Mugabe alimsimika Nelson Chamisa kugombea urais.

Chamisa ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change Alliance. Kura za awali za utafiti zilimpa 37%, ikiwa ni alama 3 tu nyuma ya Mnangagwa.

Kupitia video hiyo, Mnangagwa anasikika akiwaeleza wananchi kuwa uchaguzi huo ni kati yake na Mugabe, hivyo amewataka kuchagua mabadiliko au kubaki na maisha ya zamani.

“Sasa iko wazi kwa kila mtu kwamba Chamisa ni mtu wa Mugabe. Hatuwezi kumuamini tena kuwa nia yake ni kuleta mabadiliko Zimbabwe na kujenga upya taifa letu,” alisema Rais huyo.

“Uamuzi uko wazi, mumpigie kura Mugabe chini ya kivuli cha Chamisa au mchague Zimbabwe mpya chini ya uongozi wangu na Zanu-PF. Mabadiliko ya kweli yanakuja. Wote tunapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” aliongeza.

Zimbabwe inashiriki uchaguzi mkuu wa kwanza bila ushiriki wa Mugabe, Rais wa kwanza wa taifa hilo ambaye alilazimika kujiuzulu mwaka jana kufuatia shinikizo la wananchi wakiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mugabe amedai kuwa aliondolewa kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyosukwa na Mnangagwa pamoja na aliyekuwa mkuu wa majeshi, Constantino Chiwenga ambaye sasa ndiye makamu wa Rais.

Michael Essien awapisha vijana Black Stars
Video: Watu wanakerwa na umaarufu wangu- Haji Manara