Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru kuendelea kuchapishwa kwa gazeti la MwanaHalisi lililofungiwa kwa kipindi cha miezi 24, Septemba mwaka jana.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya HaliHalisi, Saed Kubenea amesema kuwa wamepata nakala ya hukumu ya Mahakama ambayo inaliruhusu gazeti hilo kuendelea kuchapishwa kuanzia Jumanne ya wiki ijayo.

Kupitia hukumu hiyo ya Julai 24, Mahakama Kuu imeeleza kuwa kifungo cha miezi 24 dhidi ya gazeti hilo kilichotangazwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura hakikuzingatia matakwa ya sheria.

“Tumefurahi kushinda kesi. Hukumu inaonesha kuwa hatukuvunja sheria yoyote ya habari, kwahiyo rai yangu kwa umma ni kuwa tuendelee kuiamini mahakama kwani hukumu hii inaonesha inatenda haki,” alisema Kubenea.

Hata hivyo, gazeti hilo linakutana na kiunzi kingine ambacho ni sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016, inayotaka chapisho lolote kabla halijaingia sokoni kusajiliwa ili lipate leseni.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa bado hawajapata nakala ya hukumu hiyo hivyo hawana taarifa; lakini pia hata kama MwanaHalisi wameshinda kesi hiyo hawataruhusiwa kuchapisha gazeti hadi likamilishe usajili kwa mujibu wa sheria.

“Sheria hiyo imeanza Disemba 31 mwaka 2016 ambayo inaeleza kuwa kwa namna yoyote ile hakuna gazeti litakaloruhusiwa kuchapishwa bila kuwa na leseni, basi,” alisema Dkt. Abbas.

Kwa upande wa Kubenea, amedai kuwa Mahakama pia imewataka kuhakikisha gazeti limesajiliwa kupata leseni lakini amedai litachapishwa wakati utaratibu wa kufuatilia leseni ukiendelea. Hatua hiyo huenda ikaliweka tena matatani gazeti hilo.

MwanaHalisi lilifungiwa Septemba mwaka jana kwa kile kilichoelezwa kuwa lilichapisha habari za uongo na za uchochezi.

Romeo Jozak kocha mpya Kuwait
Alichoandika Ridhiwani Kikwete baada ya Waitara, Julius Kalanga kuhamia CCM