Meneja mpya wa klabu bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich Niko Kovac amesema mshambuliaji kutoka nchini Poland Robert Lewandowski yupo kwenye mipango yake, hivyo hatokua tayari kumruhusu kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi.

Lewandowski amekua akihusishwa na taarifa za kuwa mbioni kuondoka nchini Ujerumani, huku klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid ikitajwa kuongoza katika harakati za kumsajili.

Klabu ya zamani ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 Borussia Dortmund, nayo imeonyesha nia ya kutaka kumrejesha Westfalenstadion, baada ya mtendaji mkuu Hans-Joachim Watzke kutangaza kuwa radhi kutoa hata Euro milioni 100, ili kufanikisha hatua hiyo.

Meneja Kovac amewaambia waandishi wa habari wa Ujerumani kuwa,  Lewandowski ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha FC Bayern Munich kwa misingi ya mkataba uliopo, na hatokua radhi kubariki kuondoka kwake katika kipindi hiki.

“Hakuna habari zozote mpya kumuhusu Robert, pamoja na kuwepo kwa taarifa za kuwa mbioni kuondoka, lakini ninawahakikishia hatoondoka, kwa sababu nina matarajio makubwa na mchezaji huyu kwa msimu ujao,” Alisema Kovac.

“Tunataka kufanya mambo mengi kwa msimu ujao, likiwepo suala la kutetea ubingwa wa Ujerumani, mmoja wa wachezaji mahiri ambao nitawatumia kwenye mipango ya kukamilisha tunayoyatarajia ni Robert.

“Siwezi kuzuia taarifa zinazoendelea kutolewa na vyombo vya habari kuhusu kuondoka kwa Robert, lakini mimi kama meneja nina msimamo wangu na viongozi wa juu wanafahamu kwa nini ninamzuia asiondoke katika kipindi hiki,” aliongeza meneja huyo wa zamani wa klabu ya Eintracht Frankfurt.

“Robert ana mkataba – sijui una muda gani – lakini ataendelea kuwa hapa kwa mafanikio ya klabu.”

Lewandowski anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Man Utd huko nchini Marekani, kabla ya kurejea Ujerumani tayari kwa mchezo wa kuwania German Super Cup dhidi ya Eintracht Frankfurt mwezi ujao.

Mpaka sasa mshambuliaji huyo ameshaifungia FC Bayern Munich mabao 151 kwa kipindi cha miaka minne, baada kujiunga na mabingwa hao wa Ujerumani akitokea Borussia Dortmund mwaka 2014.

Zao la Mchikichi latangazwa kuwa la Kibiashara
KCB Bank Tanzania yasaini mkataba mpya VPL