Klabu ya Leicester City ina mpango wa kumsainisha mkataba mpya beki Harry Maguire, ili kuzima ndoto za Manchester United za kutaka kumsajili katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi.

The Foxes wameshaweka msimamo wa kutokua tayari kufanya biashara ya kumuuza mchezaji huyo aliyeng’ara wakati wa fainali za kokmbe la dunia zilizomalizika nchini Urusi mwezi huu, lakini uongozi wa Man utd umeendelea kusisitiza hitaji la kumsajili Maguire.

Pamoja na mkataba wa beki huyo mwenye umri wa miaka 25 kusaliwa na miaka minne, uongozi wa Leicester City unaamini hatua ya kuongezewa mkataba mwingine mpya, huenda ukazima nzoto za Man Utd ambazo kila kukicha wamekua na mipango ya kutaka kumuhamisha King Power Stadium na kumpeleka Old Trafford.

Dhamira hiyo imekuja baada ya kukubali kumuuza kiungo mshambuliaji kutoka nchini Algeria Riyad Mahrez aliyejiunga na mabingwa wa soka nchini England Man City, kwa kwa ada ya Pauni milioni 60, hivyo hawataki kumpotza mchezaji mwingine muhimu katika kipindi hiki.

Maguire amekua na maendeleo mazuri kisoka akiwa na Leicester tangu aliposajiliwa klabuni hapo msimu uliopita akitokea Hull City kwa ada ya Pauni milioni 17.

Hali hiyo ilimuwezesha kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England iliyoshiriki fainali za kombe la dunia, na alifanikiwa kuifungia timu hiyo moja ya mabao mawili wakati wa mchezo wa robo fainali dhidi ya Sweden.

Msimu uliopita, Maguire alifanikiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Leicester City na alicheza michezo 44 ya michuano yote, huku akifunga mabao mawili, na mwishoni mwa msimu alitangazwa kuwa mchezaji bora wa klabu.

Wakati hayo yakiendelea kufanywa na viongozi wa Leicester City, dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa rasmi ndani ya majuma mawili yajayo, huku klabu hiyo ikiendelea na maandalizi ya kujiwinda na mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi Man Utd utakaochezwa Old Trafford Agosti 10.

Tukio la kupatwa kwa mwezi lisilokuwa la kawaida kutikisa Dunia
Dkt. Bashiru asema kuwanyamazisha Nape, Bashe ni kuuwa chama