Aliyekua beki wa pembeni na nahodha wa Manchester United Gary Neville, amemkosoa meneja wa klabu hiyo Jose Mourinho kwa kushindwa kumtumia kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba, katika mchezo wa jana dhidi ya Man City, ambao walichomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja.
Neville alikosoa maamuzi ya meneja huyo kutoka nchini Ureno, baada ya mpambano huo kumalizika kwenye uwanja wa Etihad mjini Manchester, kwa kusema Mourinho hakupaswa kumuweka nje ya uwanja kiungo huyo katika mchezo mgumu kama huo.
Alisema ilidhihirisha kabisa kutokuwepo kwa Pogba lilikua pigo kubwa kwa Man Utd, kutokana na uzuri wa safu ya kiungo ya Man City, ambao walihitaji kushinda mchezo wa nyumbani.
“Mourinho ni kama amejitakia kupoteza mchezo huu, sikuona mantiki yoyote ya kushindwa kumtumia Pogba, ni dhahir angecheza katika mchezo huu, eneo la kiungo lingekua na uwiyano mzuri kati ya Man Utd na Man City.”
“Kutokuwepo kwa mchezaji huyu kumesababisha mambo mengi kutokea, ukiangalia wachezaji waliochezeshwa katika nafasi ya kiungo wote wana asili ya kukaba, na ilikua mara chache sana kwao kuchezesha timu.”
“Huwezi kupambana katika mchezo mgumu kwa kuweka viungo watatu wenye sifa zinazofanana, binafsi nimeridhia kwa asilimia 100 kwa Man City kushinda mchezo huu, walistahili.” Alisema Neville aliyeitumikia Man Utd kuanzia mwaka 1992 hadi 2011.
Katika mchezo huo meneja Jose Mourinho aliamua kuwatumia viungo (Nemanja) Matic, Fellaini na (Ander) Herrera ambao wote kwa pamoja walionesha kushindwa kuhimili mikiki mikiki ya Man City wakati wote.