Gavana wa Kaunti ya Samburu nchini Kenya, Moses Lenolkulal ametofautiana na ripoti ya Wizara ya Afya iliyotolewa jana ikileza kuwa kuna visa vipya vya corona katika eneo hilo.
Akizungumza jana kwenye Hospitali ya Rufaa ya Samburu iliyoko katika Mji wa Maralal, aliwataka watu kutokuwa na hofu kwa sababu hakuna kisa chochote cha corona katika eneo hilo, bali visa vilivyotangazwa na Wizara viko katika eneo la Kaunti ya Marsabit, Forole.
“Visa vilivyoripotiwa ni kutoka Samburu, hizo sampuli zilizotumwa Nairobi hazikuwa za hapa. Tumefuatilia tumebaini kuwa sampuli zilikuwa za Forole, Marsabit na hakukuwa na sababu ya kutengeneza taharuki,” amesema.
Aliitaka Wizara na kitengo maalum cha kupambana na covid-19 kuhakikisha inaweka ipasavyo na kwa uhakika sampuli ili kuepusha taharuki.
Kenya imesharipoti visa 21,363 vya corona, wagonjwa 8,419 na watu 364 wamekufa kwa corona. Tangu Agosti 1, 2020 Serikali imeanza kulegeza masharti ikiwa ni pamoja na kufungua anga lake.