Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Prof. Benno Ndulu, amefariki dunia leo saa 10:30 alfajiri katika Hospitali ya Hubert Kairuki Memorial University alipokuwa amelazwa kwa matibabu, taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa Marehemu Mbweni JKT.
Profesa Ndulu alihudumu nafasi ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT) kuanzia mwaka 2008 – 2018.
Katibu muhtasi wake, Msafiri Nampesya ameithibitisha kutokea kifo hicho akisema bado wanafamilia na BoT wanajadiliana kuhusu mazishi yake.
Wanasiasa mbalimbali akiwemo Waziri wa Zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa zamani, Balozi Khamis Kagasheki pamoja na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo wametoa salamu za rambirambi.
Kupitia Ukurasa wake wa Twitter Waziri wa zamani, Profesa Mark Mwandosya ameandika, “Prof. Benno Ndulu, mchumi uliyebobea, mwalimu mwenzetu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umelitumikia Taifa lako #Tanzania, umeitumikia #Africa na Dunia nzima, kwa weledi wa hali ya juu. Naipa pole familia, Benki Kuu ya Tanzania, na Wana Ifakara. Pumzika kwa amani, milele. RIP.”
Mwanasiasa mwingine aliyemwomboleza Profesa Ndullu ni Waziri wa zamani, Balozi Khamis Kagasheki akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Professor Benno Ndugu, Former Governor wa Benki Kuu ya Tanzanania, Pumzika kwa Amani. #KSK_Balozi.”
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika pia katika Twitter akisema, “Sina nguvu za kusema zaidi ya Kwa Heri. Namshukuru Mola kwa kunipa nafasi ya kufanya kazi nawe kwa Miaka minane. Namshukuru Mola wetu kuwa tulionana wiki chache kabla ya umauti wako. Tangulia Prof tangulia Mchumi wetu uliyetukuka.”
Profesa Ndullu alikuwa Gavana wa Benki kuu ya Tanzania, kuanzia mwaka 2008 – 2018 na pia aliwahi kuwa mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Ndullu alizaliwa Januari 23, 1950 na amefariki akiwa na umri wa miaka 71.