Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahra Michuzi amewatoa hofu Mashabiki wa klabu ya Geita Gold FC, kufuatia adhabu ya kufungiwa kwa muda kufanya usajili kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2022/23.
Geita Gold FC imeangukiwa na adhabu hiyo kutoka Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’, kufuatia kuvunja mkataba wa Kocha kutoka nchini Burundi Etiene Ndayiragije na kushindwa kumlipa stahiki zake.
Zahra ambaye ni sehemu ya Uongozi wa Geita Gold FC, amesema tayari Uongozi wa klabu hiyo imeshapokea taarifa rasmi kutoka FIFA, na wamejipanga kulimaliza ndani ya wakati, ili adhabu iliyowakabili iondolewe haraka.
Amesema wapo tayari kumlipa Kocha Ndayiragije stahiki zake zote, na kila kitu kipo kwenye mstari, hivyo ni suala la muda, jambo hilo litakwisha na mambo mengine yataendelea.
“Suala la adhabu kupitia kwa kocha wetu tuliyeshindwa kumalizana kimkataba, tumelichukua kama funzo, na ni somo kuweza kujifunza kupitia hii adhabu, kutorejea haya makossa.”
“Niwatoe hofu mashabiki wa Geita Gold kwamba, suala hili tayari lipo katika mikono salama ya kisheria na tutakwenda kulimaliza jinsi matakwa yanavyoelekeza, tutaendelea na usajili ambao utatuwezesha kushiriki vizuri michuano ya kimataifa.” Amesema Zahra Michuzi
Ndayiragije aliajiriwa Geita Gold FC mwanzoni mwa msimu huu 2021/22, lakini kibarua chake kilisitishwa kufuatia mwenendo wa kikosi cha klabu hiyo kutoridhisha, na aliyekuwa msaidizi wake Fred Felix Minziro alikabidhiwa mikoba ya kuwa Kocha Mkuu.
Geita Gold FC kwa sasa ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na kila sababu ya kumaliza katika nafasi hiyo ama ya tatu, kutokana na mwenendo mzuri walio nao katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu.
Kama itamaliza nafasi ya tatu ama ya nne, itapata wasaa wa kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2022/23.