Mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo, George Mpole amesema anafikiria juu ya ofa alizonazo mkononi, ili afanye maamuzi wa kuondoka ama kubaki jijini Kinshasa.
Mshambuliaji huyo aliondoka Tanzania wakati wa Usajili wa Dirisha Dogo la Usajili akisajiliwa na FC Lupopo, akitokea Geita Gold FC ambayo msimu uliopita aliifungia mabao 17 na kuwa kinara wa upachikaji mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara akimuacha Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Mayele aliyefungwa mabao 16.
Mpole amesema hayo baada ya kufutwa kwa Ligi Kuu ya DR Congo msimu huu maarufu Ligue 1 huku akiwa hajacheza hata mchezo mmoja tangu atue kwenye kikosi hicho.
Mshambuliaji huyo amefafanua kuwa kinachoendelea sasa hakina afya kwenye maendeleo yake ya soka hivyo atakaporejea Tanzania ataangalia cha kufanya ili kuepukana na hilo lililomtokea sasa.
“Ligi imefutwa mpaka msimu ujao, mimi si mwenyeji huku siwezi kufahamu sana mambo yao lakini kinachotokea si kizuri kwa maendeleo yangu ya soka kwa namna ninavyohitaji kufika mbali, lazima nijue nafanyaje.”
“Nikifika huko (Tanzania), nitakuwa karibu zaidi na washauri na wasimamizi wangu tutaangalia cha kufanya, namna ya kukabiliana na hilo maana ofa zipo za nchi za nje na hata Tanzania hivyo tutajua cha kufanya,” amesema Mpole.