Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22, George Mpole huenda akaendelea alipoishia baada ya Ligi Kuu DR Congo alikokuwa akicheza kusimama kwa sababu za kiuchumi na vita.

Nyota huyo aliyekuwa akiichezea FC Lupopo, kwa sasa yupo nchini Tanzania huku klabu za Geita Gold na Tabora United zikimpa ofa ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Mpole alikuwa mfungaji bora msimu wa 2021/22, baada ya kumaliza na mabao 17 akiichezea Geita Gold, mbele ya Fiston Mayele wa Young Africans aliyekuwa na mabao 16, na kutimkia FC Lupopo ya DR Congo, kabla ya sababu za kiuchumi kuifanya ligi hiyo kusimama na Mpole kurudi Bongo.

Licha ya kwamba bado ana mkataba na Lupopo, lakini tayari timu yake ya zamani Geita Gold na Tabora United zamani Kitayosce iliyopanda Ligi Kuu msimu huu zimeonyesha nia ya kutaka kumpa mkataba baada ya kugundu ana ruhusa maalumu ya kucheza.

“Tunatafuta mshambuliaji, yupo Mpole kwa sasa na tumejaribu kuongea naye licha ya kwamba hatujafika mwafaka, kwani anatakiwa pia na timu yake ya zamani (Geita), tunazidi kusukuma usajili huu ufanikiwe licha ya kwamba utakuwa wa muda na kama ligi itarejea DR Congo itabidi arudi Lupopo,” amesema moja ya viongozi wa Kitayosce (jina tunalo). Kwa upande wake, Mpole amesema kwa sasa bado hajaamua atacheza wapi msimu ujao.

“Nikipata timu naweza kucheza ili kuendelea kutunza kiwango changu, lakini kwa sasa siwezi kusema nakwenda wapi licha ya kwamba kuna ofa ninazo,” amesema Mpole.

Sadio Mane: Nitaendelea kucheza Bayern Munich
Wizara, Taasisi zatakiwa kupunguza matumizi ya fedha