Mshambuliaji wa Geita Gold FC George Mpole ameshangazwa na taarifa za kuhusishwa kutoroka Kambini kwa shinikizo la kutaka alipwe sehemu ya fedha anayoidai klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mpole aliyemaliza Kinara wa Ufungaji Bora msimu uliopita, amesema taarifa hizo sio za kweli, lakini ni kweli yupo nje ya Kambi ya Geita Gold FC katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea.
Amesema bado ni mchezaji halali wa Geita Gold FC, na kama kuna kiongozi yoyote amelalamika katika vyombo vya habari kuhusu kutokuwepo kwake kambini, anapaswa kumtafuta ili afahamu yanayomsimu kwa sasa.
“Kiongozi gani aliyetoa taarifa kuhusu mimi? Siwezi kuzungumzia chochote kuhusu timu.Wanitafute wajue niko katika hali gani.Sina shida na kiongozi na mimi ni mchezaji halali wa Geita Gold FC.”
“Hakuna kiongozi aliyenipigia simu. Nina majeraha na najiuguza mwenyewe, ambao wanajali na kupenda uwezo wangu wananipigia simu za kunipa pole. Nimepata maumivu tulipocheza dhidi ya Coastal Union pale Tanga”
“Timu zetu zina changamoto katika matibabu. Lakini hizi ni changamoto za mpira wa Tanzania. Nashukuru naendelea vizuri.Viongozi hao wanaosema siko katika timu, ndiyo viongozi wanaosema nisiwekewe mshahara wangu, lakini kuna baadhi ya wachezaji walikaa nyumbani zaidi ya miezi miwili na walipata mishahara yao kwa wakati, sijui kwa nini kwangu imekuwa hivi. Nimefanya kazi nzuri Geita Gold, lakini sijafurahishwa nao katika hili”
“Sitamani tena kurudi kule. Najigharamia matibabu yangu na hakuna ambacho timu imekifanya katika haya matibabu. Niko nyumbani kwetu Mbeya” amesema George Mpole