Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ataendelea kununua kila goli litalofungwa na Klabu za Simba SC na Young Africans, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Rais Samia alitoa ahadi hiyo juma lililopita kabla ya timu hizo kucheza michezo ya Mzunguuko wa pili wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo Simba SC ilicheza dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco na Young Africans ilicheza dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Akihojiwa na CloudsFM Msigwa amesema, ahadi ya Rais itaendelea katika michezo inayofuata mwishoni mwa juma hili, ambapo Simba SC itakua ugenini nchini Uganda ikicheza dhidi ya Vipers SC, huku Young Africans ikikaribishwa nchini Mali dhidi ya Real Bamako.
“Kila goli litakalofungwa na Timu hizo katika mashindano ya Kimataifa litanunuliwa na Rais Samia kwa pesa ileile ya Tsh. milioni 5.”
“Tunaamini hii itaendelea kutoa hamasa kwa wachezaji wa timu zetu kuendelea kupambana kwa ajili ya taifa lao, dhumuni hapa ni kuhakikisha tunashinda ndani na nje ya nchi.” amesema Msigwa
Jumapili (Februari 19) Rais Samia alitimiza ahadi hiyo kwa kutoa shilingi milioni 15 kwa Young Africans baada ya Timu hiyo kuifunga TP Mazembe ya DR Congo 3-1, huku SImba SC ikiambulia patupu kufuatia kichapo cha 3-0 walichokipokea kutoka kwa Raja Casablanca.